Maisha ya wakimbizi wanawake na watoto
2022-06-13 10:30:00| CRI

Kila ifikapo Juni 20, dunia inaungana kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilizindua rasmi siku hii mwaka 2000, na tangu wakati huo, jamii ya kimataifa inatumia siku hii kuangalia njia za kuboresha maisha ya wakimbizi. Wengi wetu tunajua kwamba wakimbizi wanalazimika kuacha nyumba zao kwa sababu ya vita, ugaidi, au majanga mengine, lakini kukimbia kwenye nchi zao mara nyingi huwa ndio mwanzo wa safari ngumu.

Wakimbizi wengi hujikuta wakiishi katika kambi hadi wapate makazi mapya, baadhi ya makazi hayo yakiwa ni hatari au hayana vifaa vya kutosha kwa ajili ya maisha ya muda mrefu. Licha ya hayo wakimbizi siku zote huwa hawana kauli katika nchi wanazohamia, na mchakato wa urasimu katika kutafuta makazi yao mapya unaweza kuchukua miaka mingi. Migogoro ya wakimbizi duniani kote imechukua nafasi kubwa au imekuwa ikigonga vichwa vya habari katika katika miaka ya hivi karibuni, kwa hivyo ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati wowote ule kutoa msaada na kusherehekea Siku ya Wakimbizi Duniani. Katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia maisha ya wakimbizi wanawake na watoto, madhila wanayoyapitia na hata mafanikio wanayopata baadhi yao.