Mjumbe wa China ataka Baraza la Usalama la UM kurekebisha vikwazo vya Sudan
2022-06-22 09:29:25| CRI

Mshauri wa Tume ya Kudumu ya China katika Umoja wa Mataifa Bw. Xing Jisheng amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurekebisha vikwazo nchini Sudan kwa wakati muafaka, huku eneo la Darfur nchini Sudan likiwa lipo katika hatua muhimu ya kuhama kutoka ulinzi wa amani hadi ujenzi wa amani.

Akizungumzia hali ya usalama katika mkoa wa Darfur, Bw. Xing amebainisha kuwa kwa ujumla hali ni shwari, lakini bado ni tete, huku matukio ya vurugu, ikiwa ni pamoja na mapigano kati ya jamii, yanatokea mara kwa mara.

Ameongeza kuwa baada ya kuondolewa kwa Tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mjini Darfur, serikali ya Sudan inachukua jukumu la msingi la ulinzi wa raia. Hivyo amesema kwa kuzingatia hali inayoendelea, Baraza la Usalama linapaswa kurekebisha vikwazo vya Sudan kwa wakati, na kuunda mazingira mazuri kwa serikali ya Sudan kuimarisha uwezo wake wa kulinda raia.

Bw. Xing amesisitiza kuwa azimio nambari 2620 la Baraza la Usalama linatoa wito wa kuanzishwa kwa vigezo vilivyo wazi, vilivyofafanuliwa vizuri na halisi vya kurekebisha vikwazo vya Sudan ifikapo tarehe 31 mwezi Agosti, na China inatumai linaweza kutekelezwa kwa wakati.