China yasimama kidete katika kuendelea kuunga mkono amani endelevu, usalama, na maendeleo katika pembe ya Afrika
2022-06-22 09:32:57| CRI

Mjumbe maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China katika pembe ya Afrika, Bw. Xue Bing amesisitiza azma ya China ya kuendelea kuunga mkono nchi za Pembe ya Afrika (HOA) katika juhudi zao za kuwa na amani endelevu, usalama na maendeleo.

Bw. Xue ameyasema hayo wakati Mkutano wa kwanza wa Amani, Utawala Bora na Maendeleo kati ya China na nchi za Pembe ya Afrika ukianza Jumatatu. Akiongea na mawaziri na maafisa waandamizi waliohudhuria mkutano huo jijini Addis Ababa, Ethiopia, Bw. Xue amesisitiza kuwa China itaendelea kuziunga mkono nchi hizo kudumisha mtazamo wa pamoja, mpana, ushirikiano na usalama endelevu; kulinda amani na usalama wa kikanda; na kunyamazisha silaha katika Pembe ya Afrika.

Wakati huohuo mjumbe huyo wa China ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza uwekezeji wao na kuchangia pakubwa katika uhuru na maendeleo endelevu ya kanda hiyo na Afrika kwa ujumla.

Mkutano huo wa siku mbili uliomalizika Jumanne, uliwaleta pamoja mawaziri na wawakilishi wa ngazi ya juu wa nchi za Pembe ya Afrika zikiwemo Ethiopia, Kenya, Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Uganda na Djibouti.