Tetemeko la ardhi la Afghanistan lasababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000
2022-06-23 09:13:47| CRI

Mkurugenzi wa idara ya habari na utamaduni wa Afghanistan Bw. Mohammad Amin Haddifa amesema kuwa tetemeko la ardhi lililotokea mashariki ya nchi hiyo jana mapema na kufuatiwa na maporomoko ya udongo katika wilaya mbili za Gayan na Barmal za Paktika limesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000, na wengine zaidi ya 1,500 kujeruhiwa, ambapo idadi ya waliopoteza maisha huenda ikaongezeka zaidi.

Katika jimbo jirani la Khost, watu karibu 25 walifariki na wengine 100 kujeruhiwa baada ya nyumba, misikiti na maduka zaidi ya 600, kuharibiwa na tetemeko hilo.

Baada ya tetemeko hilo, Kaimu Waziri Mkuu Mullah Mohammad Hassan Akhund aliongoza kikao cha dharura cha baraza la mawaziri, na kuamuru kutolewa ruzuku ya dola za kimarekani zaidi ya milioni 11.2 ili kusaidia wahanga.

Mkutano huo umeagiza pande zote husika kukimbilia mahali pa tukio mara moja, na kutumia rasilimali zote zilizopo kuokoa maisha ya watu walioathirika na kutoa misaada yote muhimu.

Tetemeko hilo lenye kiwango cha rechta 5.9 lilitikisa kilomita 44 kusini magharibi mwa Khost.