Rais Xi aongoza mkutano wa 14 wa BRICS akihimiza umuhimu wa ushirikiano ulio bora zaidi
2022-06-24 09:35:58| CRI

Rais Xi Jinping wa China ameongoza mkutano wa 14 wa BRICS jana Alhamis hapa Beijing, ambao ulifanyika kwa njia ya mtandao wa internet. Wakuu wa nchi za BRICS wakiwa ni pamoja na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, rais wa Brazil Jair Bolsonaro, wa Russia rais Vladimir Putin na waziri mkuu wa India Narendra Modi wameshiriki kwenye mkutano huo. Kwa maelezo zaidi huyu hapa…..

Akiwa mwenyeji wa mkutano huo kwanza rais Xi Jinping alitoa hotuba ya kuwakaribisha wageni wake, akisema kwa zaidi ya mwaka mmoja, licha ya mazingira ya kuogopesha na magumu, nchi za BRICS zimeendelea kuwa na moyo wa BRICS wa uwazi, ujumuishi na ushirikiano wa kunufaishana, kuongeza mshikamano na ushirikiano na kukabiliana kwa pamoja na ugumu.

“Mfumo wa BRICS umeonesha uthabiti na uhai. Ushirikiano wa BRICS umepata maendeleo na matokeo makubwa. Mkutano huu unafanyika katika wakati muhimu wa kujenga mustakbali mzuri wa binadamu. Nchi za BRICS, zikiwa kama soko muhimu linaloibukia na nchi kubwa zinazoendelea, zinahitaji kufanya kazi kwa uwajibikaji, kuongea kwa usawa na haki, kuendelea kuwa imara zikiwa na imani kwamba janga litashindwa, kuongeza nguvu kwa ajili ya ufufukaji wa uchumi, kutetea maendeleo endelevu, kuchangia mawazo na busara kwa ajili ya maendeleo yaliyo bora zaidi ya ushirikiano wa BRICS pamoja na kutoa nguvu chanya, tulivu na ya kiujenzi duniani.”

Katika mkutano huo ambao rais Xi alitoa hotuba muhimu yenye kichwa kisemacho “Kuhimiza Ushirikiano ulio Bora zaidi na Kukumbatia njia mpya ya Ushirikiano wa BRICS”, amesema China inapenda kushirikiana na nchi za BRICS kuendesha Mpango wa Usalama Duniani (GCI), kutetea wazo la pamoja, la kina, ushirikiano na usalama endelevu, kuanzisha njia mpya ya usalama ambayo itakuwa ya majadiliano na sio makabiliano, ushirikiano mzuri na sio ushirikiano mbaya, na pande zote kunufaishana na sio kunufaisha upande mmoja, pamoja na kuleta utulivu zaidi na nguvu chanya duniani.

Mbali na hapo rais Xi pia amesisitiza kwamba China ipo tayari kushirikiana na nchi za BRICS kuongeza uhai zaidi katika Mpango wa Maendeleo Duniani (GDI), kuupa nguvu utekelezaji wa ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030, kujenga jumuiya ya maendeleo duniani na kuchangia kwenye maendeleo yenye nguvu, kijani na mazuri duniani.

Amebainisha kuwa wanachama wa BRICS wameongeza kasi ya kujenga Ushirikiano wa BRICS na kuwa Uvumbuzi Mpya wa Viwanda, kufikia Mfumo wa Ushirikiano wa Uchumi wa Kidijitali na kutangaza Mpango wa Ushirikiano wa Utengenezaji wa Kidijitali.

Hivyo ameziambia nchi wanachama kwamba ni muhimu kuboresha mchakato wa kupanua wanachama wa BRICS mapema zaidi, kwani itaongeza ushirikiano zaidi na uwakilishi na ushawishi wa BRICS.

“Tukiwa kama wawakilishi wa soko linaloibukia na nchi zinazoendelea, ni lazima tutoe maamuzi sahihi na kuchukua hatua za kuwajibika katika wakati muhimu wa kihistoria. Tunachofanya kitakuwa na matokeo muhimu duniani. Wacha tuungane pamoja, kuongeza nguvu na kusonga mbele katika kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja na kujenga mustakabali mzuri kwa binadamu.”

Chini ya kauli mbiu ya“Kuhimiza Ushirikiano ulio Bora zaidi na Kukumbatia njia mpya ya Ushirikiano wa BRICS”, viongozi wa nchi tano walibadilishana mawazo kwa kina juu ya ushirikiano wa BRICS katika sekta mbalimbali na masuala makubwa wanayoyafuatilia kwa pamoja na kufikia makubaliano muhimu.

Wamekubaliana juu ya haja ya kukabiliana kwa pamoja na UVIKO-19, kutoa mfumo kamili kama vile kituo cha kutafiti na kuzalisha chanjo cha BRICS, kuhimiza ugawaji sawa na wa haki wa chanjo, na kuboresha maandalizi wanapokabiliwa na misukosuko ya afya ya umma. Azimio la Mkutano wa BRICS wa Beijing lilipitishwa na kutolewa kwenye mkutano huo.