Mkutano wa G7 wafunguliwa licha ya matarajio duni na maandamano
2022-06-27 08:38:07| CRI

Viongozi wa Kundi la Nchi Saba (G7) wameanza mkutano wao wa siku tatu wa kila mwaka mjini Schloss Elmau, nchini Ujerumani, licha ya maarajio hafifu ya matokeo ya mkutano huo na maandamano.

Mkutano huo unatarajiwa kuzungumzia mgogoro wa Russia na Ukraine, mabadiliko ya tabianchi, na maswala mengine.

Mgogoro wa Russia na Ukraine, hususan vikwazo dhidi ya Russia, unatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mkutano huo, huku rais wa Marekani Joe Biden akisema jana kuwa, Kundi hilo litaweka vizuizi vya uagizaji wa dhahabu kutoka Russia.

Kwa mujibu wa Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, katika siku ya kwanza ya mkutano huo, viongozi wa nchi wanachama wa Kundi hilo watajadili masuala ya uchumi wa dunia yatakayohusiana na migogoro inayokabili jamii ya kimataifa kwa sasa, ikiwemo kushuka kwa ukuaji wa uchumi wa baadhi ya nchi, kuongezeza kwa gharama za maisha, upungufu wa malighafi na kuvurugika kwa mnyororo wa ugavi.

Hata hivyo, watu 4,000 waliandamana mjini Munich kupinga mkutano huo, huku baadhi ya waandamanaji wakizilaumu nchi kubwa za Magharibi kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine, na kusababisha dunia nzima kubeba mzigo wa matokeo ya mgogoro huo, ikiwemo mgogoro wa chakula.