FAO, OECD zaonya juu ya changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo na chakula duniani
2022-06-30 08:41:28| CRI

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) zimeonya juu ya changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo na chakula katika muongo mmoja ujao.

Katika ripoti yao ya pamoja inayoitwa “Mtazamo wa Kilimo kwa mwaka 2022-2031” iliyotolewa jana, mashirika hayo yamesema, sekta ya kilimo na chakula inahitaji kulisha idadi ya watu inayoongezeka katika njia ambayo ni endelevu. Pia ripoti hiyo imesema, sekta hiyo inatakiwa kushughulika na athari za mabadiliko ya tabianchi na athari za kiuchumi na kuvurugika kwa upatikanaji wa chakula kutokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine.

Ripoti hiyo imesema, katika nchi za kipato cha chini na cha kati, mahitaji ya chakula yataendelea kuongezeka ikilinganishwa na nchi zenye kipato cha juu, ambako mahitaji yatadhibitiwa na ongezeko la taratibu la idadi ya watu.