Umuhimu wa vyama vya ushirika kwa wanawake
2022-06-30 10:49:50| CRI

Kama alivyosema Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania TFC Theresia Alex Chitumbi ni kwamba Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika ya Umoja wa Mataifa (UM) huadhimishwa kila ifikapo Jumamosi ya kwanza ya mwezi Julai kila mwaka tangu mwaka 1923. Baadhi ya malengo ya siku hiyo ni kuongeza uelewa juu ya vyama vya ushirika, pamoja na kuimarisha na kupanua ushirikiano kati ya jumuiya ya kimataifa ya vyama vya ushirika na mashirika mengine yanayounga mkono zikiwemo serikali.

Vyama vya ushirika duniani kote vinaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika kwa njia nyingi. Shughuli zinazofanywa ni pamoja na: ujumbe kutoka Muungano wa Kimataifa wa Vyama vya Ushirika (ICA) na Umoja wa Mataifa zinazotafsiriwa kwa lugha za kienyeji ili kusambazwa kote duniani, makala za habari na vipindi vya redio vinavyotangaza ufahamu wa siku hiyo, maonesho, mashindano na kampeni zinazozingatia mada zinazohusiana na siku hiyo, mikutano na maafisa wa serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine washirika; changamoto za kiuchumi, kimazingira, kijamii na kiafya (kama vile upandaji miti), na kufadhili matukio ya kitamaduni kama vile sinema na matamasha. Hivyo basi leo hii tutaangalia Vyama vya Ushirika na vile vinavyowanufaisha wadau wake hasa wanawake.