Waziri wa mambo ya nje wa China afafanua msimamo wa China kuhusu suala la Myanmar
2022-07-04 08:54:23| CRI

Waziri wa mambo ya nje Bw. Wang Yi ambaye yuko ziarani nchini Cambodia, jana jumapili alibadilishana maoni na naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Prak Sokhonn kuhusu suala la Myanmar.

Bw. Prak Sokhonn ambaye pia ni mjumbe wa Umoja wa Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) kwa Myanmar, alimwelezea Bw. Wang Yi kuhusu ziara yake nchini Myanmar. Bw. Wang ameipongeza Cambodia ikiwa mwenyekiti wa zamu wa ASEAN kwa mwaka 2020, katika upatanishi wa suala la Myanmar, na pia amefafanua msimamo wa China kuhusu suala hilo.

Bw. Wang amesema, kwanza, China inatarajia juhudi za pamoja za China na ASEAN katika kutafuta maafikiano ya kisiasa kati ya pande zote za nchi hiyo kwa mujibu wa katiba na sheria; Pili, inataka kushirikiana na ASEAN kuanzisha upya mchakato wa mpito wa kidemokrasia nchini Myanmar na kutafuta njia ya maendeleo ya kisiasa inayoifaa nchi hiyo; Tatu, inatarajia ASEAN kufuata “Njia ya ASEAN” ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, na kufanya kazi za kiujenzi ili kulinda mshikamano wa ASEAN na hadhi yake ya uongozi.