Watu tisa wafariki kwa ajali ya barabarani nchini Uganda
2022-07-11 10:32:05| CRI

Watu tisa wamefariki na wengine watano kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea katika wilaya ya Luweero katikati ya Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyotolewa Jumamosi, ajali hiyo ilitokea baada ya gari la usafiri wa umma aina ya van kugongana na lori, ambapo inadaiwa kuwa gari hilo lililokuwa likitoka Kampala kuelekea Gulu lilikuwa likiendeshwa kwa kasi na kusababisha tairi lake la nyuma kupasuka, na kufanya dereva kushindwa kulidhibiti na hatimaye kupinduka mara kadhaa kabla ya kugongana na lori lililokuwa likija mbele yake. Abiria waliokufa na kujeruhiwa wote walikuwa kwenye van.

Kulingana na takwimu za polisi, kila mwaka zinatokea ajali 20,000 za barabarani na kusababisha zaidi ya watu 2,000 kufariki na kuifanya Uganda kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vikubwa zaidi vya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.