China na Marekani zahimizwa kuwa na maingiliano mazuri katika eneo la Asia na Pasifiki
2022-07-12 10:28:19| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema China na Marekani zinapaswa kuwa na maingiliano mazuri katika eneo la Asia na Pasifiki.

Wang alisema hayo alipoulizwa kuhusu jaribio la Marekani na mataifa mengine kutaka kuimarisha na kupanua uwepo na ushawishi wao katika eneo hilo, wakati alipokuwa akitoa hotuba ya sera na kujibu maswali katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN.

Wang alisema, China siku zote iko wazi kwa ushiriki wa mataifa mengine katika masuala ya Asia na Pasifiki, na kuongeza kuwa, cha msingi ni kujua kama hatua zao zinasaidia kudumisha amani na utulivu wa kikanda, au kujaribu kuzusha mivutano na makabiliano; ni kukuza maendeleo na ufufuaji wa kikanda, au kutafuta utengano na kuvunja uhusiano; ni kuimarisha umoja na ushirikiano wa kikanda, au kujaribu kutumia njia zao wenyewe au hata kuleta migawanyiko.

Alisema inaaminika kuwa watu katika nchi zote za eneo hilo watakuwa na uamuzi wao wenyewe, na historia itafanya tathmini ya haki juu ya hili.