Maendeleo makubwa yapatikana katika elimu ya juu kwa wasichana
2022-07-12 14:39:54| CRI

Katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni wanafunzi wengi wanaojiandaa kuingia chuo kikuu wanakuwa wameshafanya mitihani yao ya kumaliza na wengi wao wanakuwa wamepata matokeo ya mtihani. Kadiri miaka inavyosonga mbele ndivyo inaonekana kwamba maendeleo ya elimu kwa wanawake yanazidi kuwa makubwa na kuleta fahari isiyo na kifani kwa wanawake wengi ambao huko nyuma walikuwa wakisahauliwa sana kielimu na kuonekana kana kwamba wao hatima yao ni kuhudumia mume, watoto na nyumba tu.

Kitu chochote kile ukikifanya kwa bidii na maarifa, matunda yake huonekana bila kificho, na juhudi za wasichana hawa za kuondoa dhana hii ambayo tunaweza kusema kuwa ni potofu kabisa zimezaa matunda, kwani mwaka huu wasichana wameonesha maajabu makubwa katika matokeo yao ya kuingia chuo kikuu. Hivyo ili kuthamini juhudi za wasichana hawa leo katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutakuletea habari njema zinazowahusu wanawake ambao wamefanya vizuri kwenye mitihani yao ya kuingia chuo kikuu na kumaliza kidato cha sita.