OCHA yaeleza wasiwasi juu ya mauaji ya raia mashariki mwa DRC
2022-07-14 11:10:59| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeeleza wasiwasi wake juu ya mauaji ya takriban watu 31 ndani ya wiki moja katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

OCHA ilisema raia 11 waliuawa na 57 kutekwa nyara, wakiwemo watoto wapatao 30 katika mashambulizi dhidi ya vijiji vya eneo la Irumu katika mkoa wa Ituri wakati wa Julai 7-12. Imeongeza kuwa nyumba 600 pia zilichomwa moto na washirika wa mambo ya kibinadamu wa nchi hiyo wanakadiria kuwa watu 24,000 walikimbilia vijiji jirani. Takriban raia watano waliuawa siku ya Jumanne wakati makundi yenye silaha yaliposhambulia mji wa Beni huko Kivu Kaskazini. Katika shambulizi jipya lililotokea katika kituo cha afya huko Beni, raia 15 akiwemo mhudumu wa afya na wagonjwa, waliuawa na wengine kadhaa kutekwa nyara. Hili lilikuwa shambulizi la nane dhidi ya kituo cha afya huko Kivu Kaskazini mwaka huu.

OCHA imesema mashambulizi hayo yanakuja wakati mapigano kati ya jeshi la DRC na kundi la waasi la M23 yanaendelea katika eneo la Rutshuru huko Kivu Kaskazini, na kwamba takriban watu laki saba wamekimbia makazi yao nchini humo mwaka huu, na kufanya jumla ya wakimbizi wa ndani kufikia zaidi ya milioni 6.