Mapigano kati ya kundi la M23 na jeshi la DRC yasababisha uhamaji mkubwa wa watu
2022-07-15 09:31:52| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika taarifa yake kuwa mapigano ya hapa na pale kati ya jeshi na waasi wa kundi la waasi la M23 yaliendelea katika eneo la Rutshuru, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, na kusababisha uhamaji mkubwa wa watu.

Tangu mwishoni mwa Machi 2022, kundi la M23 limekuwa likifanya mashambulizi katika jimbo la Kivu Kaskazini, kaskazini mashariki mwa DRC, na vitongoji kadhaa vya jimbo hilo sasa vipo mikononi mwa waasi hao kwa wiki kadhaa.

Kwa mujibu wa OCHA, hadi kufikia Julai 8, maeneo ya afya ya Rutshuru na Rwanguba katika jimbo la Kivu Kaskazini yalikuwa yamepokea zaidi ya watu 124,000 waliokimbia makazi yao.

Aidha, shughuli za kijamii na kiuchumi zinaendelea kulemazwa huko Bunagana katika eneo la Rutshuru, mwezi mmoja baada ya kukaliwa na kundi la M23 Juni 12.