Umoja wa Mataifa watoa wito wa kubadili fikra ili kutimiza lengo la maendeleo la Afrika
2022-07-21 08:38:32| CRI

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina Mohammed amesema, lengo la kijasiri la maendeleo la Afrika bado linaweza kutimia, na kutimizwa kwake kunahitaji mabadiliko ya fikra na kubadili mgogoro kuwa fursa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja huo kwenye mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu ya Afrika, Bi. Mohammed amesema, mafanikio ya maendeleo katika bara la Afrika yako hatarini, kama matokeo ya migogoro mitatu inayoendelea sasa duniani, ambayo ni janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na vita inayoendelea nchini Ukraine.

Ametaja mambo matano muhimu ili kubadili fikra kuwa fursa, ambayo ni kutunga mipango na sera sahihi na kujenga taasisi imara, kujenga miundombinu ya kisasa kwa Afrika kwa kuwekeza katika maingiliano na teknolojia ya kidijitali, kuzingatia elimu na maendeleo ya ujuzi ili kuwezesha mageuzi ya kiviwanda barani Afrika, kutimiza nishati endelevu kwa wote barani humo, na mtazamo wa pamoja kuhusu ufadhili.