Tatizo la macho kwa watoto
2022-07-21 15:42:29| CRI

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watoto wengi siku hizi wanapenda kutumia vifaa vya kisasa kama vile simu za viganjani, tablet na computer kucheza michezo ya kwenye simu. Hili si jambo baya sana, lakini linaleta tatizo lingine, ambalo ni ugonjwa wa myopia, ambapo mtoto anaweza kuona vitu vya karibu, lakini hawezi kuona mbali.

Tatizo hili limekuwa sugu kwa watoto wengi, maana hufurahia sana michezo hiyo ya kwenye simu na matokeo yake ni kwamba, wanakosa mwanga wa jua, ambao ni muhimu sana, na hivyo kuwasababishia tatizo hilo la macho. Tatizo lingine linalowakabili watoto katika zama hizi ni saratani ya jicho. Asilimia 80 ya watoto wenye umri wa kati ya mwaka mmoja hadi miaka mitano wanaougua saratani ya jicho nchini Tanzania wanafariki kila mwaka kutokana na kuchelewa kupata matibabu, kwani saratani hiyo inatibika. Kutokana na matatizo hayo, katika kipindi chetu leo tutazungumzia tatizo la myopia kwa watoto, na pia saratani ya jicho kwa watoto.