Watu mashuhuri wa Afrika: “Mtego wa Madeni” unaosisitizwa na nchi za Magharibi ni kauli potoshi
2022-07-22 15:40:11| CRI

“Unaoitwa ‘mtego wa madeni’ unaodaiwa kuchangiwa na pendekezo la ‘Ukanda Mmoja, Njia Moja’ la China ni kauli potoshi ya nchi za Magharibi yenye lengo la kuipaka matope China. Kwa nchi za Afrika mambo haya sio ya kiujenzi, na wanatutaka tu tupoteze fursa nyingi kwenye mambo hayo.” Alisema Rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Alberto Chissano alipotoa hotuba kwa njia ya video kwenye Sehemu ya Kwanza ya Mkutano wa 11 wa Baraza la Jumuiya za Washauri Bingwa la China na Afrika uliofanyika Julai 21 huko Jinhua mkoani Zhejiang.

 Sehemu ya Kwanza ya Mkutano wa 11 wa Baraza la Jumuiya za Washauri Bingwa kati ya China na Afrika ilifanyika kwa njia mseto ya video na ana kwa ana, ambapo wajumbe kutoka China na nchi nyingi za Afrika wamefanya majadiliano ya kina kuhusu Pendekezo la “Ukanda Moja, Njia Moja” na ushirikiano wa kifedha kati ya China na Afrika kwa ajili ya maendeleo. Hivi karibuni, kufuatia Kundi la Nchi Saba (G7) kutangaza kuzindua mpango wa kuendeleza miundombinu duniani, baadhi ya nchi za Magharibi zimeongeza nguvu katika kuichafua pendekezo la “Ukanda Moja, Njia Moja”. Katika hali hiyo wajumbe kutoka nchi nyingi za Afrika waliohudhuria mkutano huo wamekanusha lawama zao zisizo na msingi.

Bw. Chissano amesema, kauli potoshi zilizotolewa na nchi za Magharibi zinazodai kuwa pendekezo la “Ukanda Moja, Njia Moja”litaziingiza nchi za Afrika kwenye eti “mtego wa madeni”, lakini ukweli ni kwamba miradi yote ya miundombinu haikuamuliwa au kuchaguliwa na upande wa China, bali ni miradi inayohitajika kwa ajili ya maendeleo ya Afrika. Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika pia imesisitiza hitaji kubwa la Afrika kwenye maendeleo ya miundombinu. Bw. Chissano amesema, mwanzoni nchi zilizoendelea zote hazitaki kuwekeza kwenye miundombinu barani Afrika, na ni China tu iliyojitokeza kuzisaidia nchi za Afrika. Si kama tu kwenye nyanja ya miundombinu, China pia imekuwa ikitoa fedha na teknolojia kuzisaidia nchi za Afrika kuondoa vizuizi kwenye maendeleo ya uchumi na jamii, na kutoa uungaji mkono mkubwa kwenye sekta ya viwanda, kilimo cha kisasa, biashara, uwekezaji na afya ya umma na kadhalika.

Balozi wa Guinea-Bissau nchini China Antonio Serifo Embalo amesema, katika miaka ya hivi karibuni chini ya mfumo wa “Ukanda Moja, Njia Moja”, Afrika na China zimeharakisha mchakato wa ushirikiano kati yao kwenye pande zote kuanzia utamaduni hadi mavumbuzi ya sayansi na teknolojia, na hadi uchumi wa kijani. Ushirikiano kati ya Afrika na China chini ya “Ukanda Moja, Njia Moja” umeweka mfano wa kuigwa wa aina mpya ya ushirikiano wa kimataifa, ambao umesukuma mbele maendeleo ya dunia kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Mfuko wa Jadeas Trust wa Nigeria Bibi Yetunde Aina pia amekanusha kauli potoshi zilizotolewa na nchi za Magharibi zinazolishutumu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kuchangia “Mtego wa Madeni” Afrika. Bibi Aina anaona, uhusiano kati ya Afrika na China unapaswa kusimuliwa na waafrika na wachina wenyewe. Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa usalama, ukosefu wa ajira, kushuka thamani kwa sarafu na ukosefu wa fedha kwa ajili ya miundombinu, ambazo zinatatuliwa hatua kwa hatua chini ya uungaji mkono wa China na washirika wengine wa kimataifa.

Sehemu ya Kwanza ya Mkutano wa 11 wa Baraza la Jumuiya za Washauri Bingwa la China na Afrika iliandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang na serikali ya mji wa Jinhua wa mkoa wa Zhejiang.