Kampuni za China na chuo kikuu cha Uganda kuimarisha ushirikiano katika mafunzo
2022-07-22 08:34:15| CRI

Kampuni za China kupitia Shirikisho la Wafanyabiashara wa China nchini Uganda zimesaini makubaliano ya awali na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda katika juhudi za kuimarisha mafunzo ya vipaji na ajira.

Kaimu mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Barnabas Nawangwe na mwakilishi wa Shirikisho hilo Zheng Biao walisaini makubaliano hayo katika Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala.

Nawangwe amesema Chuo Kikuu cha Makerere ni moja ya vyuo vikuu bora zaidi barani Afrika, na kulishukuru Shirikisho la Wafanyabiashara wa China nchini Uganda kwa kukiunga mkono.

Kwa upande wake, Zheng amesema elimu ni tumaini la maendeleo katika nchi yoyote, na kuongeza kuwa, watatafiti njia za kutimiza ujuzi wa ujasiriamali na kupanua mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na kuandaa wafanyakazi wenye ubora wa juu wanaoweza kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.