Marekani yashindwa kuzishawishi nchi za Mashariki ya Kati kuipinga China
2022-07-22 09:26:29| CRI

Tangu rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aanzishe mvutano na China, wakati maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani wanapofanya ziara katika nchi za nje, jambo ambalo wote hawaachi kulifanya ni kuzishawishi nchi hizo kushirikiana na Marekani kuipinga China. Katika ziara yake Mashariki ya Kati hivi karibuni, rais Joe Biden wa Marekani pia hakusahau kufanya hivyo, lakini alishindwa kwa mara nyingine tena.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya Marekani na vyombo vya habari, lengo kuu la ziara hiyo ya Biden ni kuzishawishi nchi za Mashariki ya Kati kuongeza uzalishaji wa mafuta, ili kuisaidia Marekani kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei nchini humo. Lengo lingine la kimkakati la ziara hiyo, ni kuzishawishi nchi hizo kuipinga China, na kukataa ushawishi wa China katika eneo hilo ambao unaongezeka kwa kasi.

Saudi Arabia ni nchi muhimu ya Mashariki ya Kati, hivyo kuilazimisha “kuchagua moja kati ya China na Marekani” ni moja ya madhumuni makuu ya ziara ya rais Biden nchini humo. Kabla ya ziara hiyo, rais Biden alichapisha makala katika gazeti la The Washington Post, akisisitiza umuhimu wa Saudi Arabia, na kusema hivi sasa kazi yake muhimu ni kuifanya Marekani iwe na mazingira bora zaidi ili kupingana na China. Hata hivyo, Saudi Arabia imekataa wazi kuungana na Marekani kupinga China. Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Adel Al-Jubeir amesema, uhusiano wa Saudi Arabia na Marekani na uhusiano wake na China hauingiliani, na Saudi Arabia itaendelea kudumisha uhusiano mzuri na Marekani na China kwa wakati mmoja. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan Al Saud alipohojiwa na Kituo cha CNN cha Marekani hivi karibuni, alisema anapinga maoni kuwa China ni adui, na kile kinachohitajika na Saudi Arabia, Mashariki ya Kati na dunia ni ushirikiano, na sio mvutano.

Maoni ya Saudi Arabia kuhusu uhusiano na China unawakilisha nchi nyingine nyingi za Mashariki ya Kati. Katika miaka mingi iliyopita, ili kupata maslahi zaidi za kisiasa, kiuchumi na kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati, Marekani imeiletea eneo hilo maumivu mengi, kwa kuchochea vurugu, vita, na mapinduzi ya kupindua serikali. Wakati huohuo, China imefanya ushirikiano wa kunufaishana na nchi za Mashariki ya Kati,  bila kuzifundisha jinsi ya kutawala, au kuvamia nchi yoyote. Kabla ya  ziara ya rais Biden, nchi kadhaa za Mashariki ya Kati zikiwemo Saudi Arabia, Iran na Misri zilitangaza nia ya kujiunga na utaratibu wa ushirikiano wa BRICS. Moja ya madhumuni yao ya kufanya hivyo ni kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na China.

Katika ziara yake, rais Biden amedai kwamba Marekani haitaondoka, ili isiache nafasi kwa China, Russia na Iran katika Mashariki ya Kati. Kauli hiyo inaonesha umwamba wa Marekani, kwani Mashariki ya Kati sio uani kwa Marekani, na haitaki kupinga nchi nyingine ili kufurahisha Marekani.