Waziri wa mambo ya nje wa Russia afanya ziara nchini Misri
2022-07-25 08:47:28| CRI

Rais wa Misri Abef-Fattah al-Sisi amefanya mzungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov aliyeko ziarani nchini humo, katika mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili uhusiano wa pande mbili na masuala ya kikanda na kimataifa yanayofuatiliwa na pande hizo mbili.

Rais al-Sisi alisifu ushirikiano unaokua kati ya Misri na Russia, uliodhihirishwa na miradi mbalimbali ya Russia nchini Misri, ikiwemo kituo cha nyuklia cha El-Dabaa ambacho kinaendelea kujengwa, na kuanzishwa kwa Kanda ya Viwanda vya Russia katika ukingo wa Mfereji wa Suez.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Misri imesema, waziri Lavrov amemkabidhi rais al-Sisi barua kutoka kwa rais wa Russia, Vladmir Putin, akieleza umuhimu ambao Russia imeweka katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Misri ndani ya mfumo wa makubaliano ya uhusiano na ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia barani Afrika tangu kuanza kwa mgogoro kati ya nchi hiyo na Ukraine mwezi Februari mwaka huu.