Jumba la Makumbusho ya Maswasiliano kati ya China na Afrika laweka jukwaa jipya la kusimulia urafiki wa China na Afrika
2022-07-26 09:26:07| CRI

Tarehe 21 mwezi Julai, mradi wa ujenzi wa Jumba la Makumbusho ya Mawasiliano kati ya China na Afrika ulizinduliwa rasmi kwenye kongamano la kwanza la Mkutano wa 11 wa Baraza la Jumuiya za Washauri Bingwa la China na Afrika. Jumba hilo la makumbusho, likiwa ni  la ujenzi wa kipindi cha pili wa  mradi wa Jumba la Makumbusho la Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, linatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwaka huu baada ya ujenzi kukamilika.

Jumba la Makumbusho ya Mawasiliano kati ya China na Afrika si kama tu litaonesha historia ya zaidi ya miaka elfu mbili ya mawasiliano kati ya pande hizo mbili, bali pia litafafanua kwa undani maingiliano kati ya pande hizo mbili kwenye sekta mbalimbali zikiwemo muziki na dansi, Kongfu, elimu, mtandao wa reli, afya, matibabu na kilimo. Mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang Prof. Yoro Diallo, ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Jumba la Makumbusho la Afrika katika chuo kikuu hicho, amesema kuwa uzinduzi wa mradi wa Jumba la Makumbusho ya Mawasiliano kati ya China na Afrika ni hatua nyingine muhimu kwenye uhusiano kati ya Afrika na China, na una umuhimu mkubwa kwa watu wa Afrika, kwa kuwa unaweza kuimarisha maingiliano ya kiutamaduni kati ya pande hizo mbili.

Baada ya ujenzi kukamilika, Jumba hilo litashirikiana na kukamilishana na Jumba la Makumbusho ya Ustaarabu wa China na Afrika ambalo ni la ujenzi wa kipindi cha kwanza cha mradi huo, na kuwa mstari wa mbele wa diplomasia kati ya watu wa China na Afrika, pia ni jukwaa jipya la kusimulia urafiki kati ya pande hizo mbili. Imefahamika kuwa, Jumba la Makumbusho la Afrika ni la kwanza la aina yake katika vyuo vikuu vya China,  jumba la ujenzi wa kipindi cha kwanza cha  mradi wake  lilifunguliwa mwezi Oktoba mwaka 2010, na mpaka sasa limepokea watazamaji zaidi ya laki moja.