Shirika la Kibinadamu la Umoja wa Mataifa laomba fedha za dharura kuepuka mgogoro wa chakula katika Pembe ya Afrika
2022-07-26 08:23:34| CRI

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UNOCHA) imeomba msaada wa dharura wa fedha ili kusaidia kuepuka janga la kibinadamu linalotishia Pembe ya Afrika kufuatia ukame mkali.

Katika ripoti yake iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya, Ofisi hiyo imesema endapo fedha hizo hazitapatikana, watu wengi watapoteza maisha yao.

Ripoti hiyo imesema watu katika Pembe ya Afrika, hususan nchi za Kenya, Ethiopia na Somalia, wanaoteseka na ukame mbaya zaidi kutokea katika miaka 40 iliyopita, wanakabiliwa na tishio la njaa kufuatia misimu minne mfululizo ya uhaba wa mvua.

Shirika hilo limesema, watu milioni 19.4 wameathiriwa na ukame ulioanza mwezi Oktoba, 2020 katika kanda hiyo, na kuongeza kuwa watu milioni 18.6 katika nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia wanakabiliwa na hali mbaya ya usalama wa chakula na ukosefu wa lishe bora, na kuonya kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia watu milioni 20 itakapofika mwezi Septemba.