Rais wa China akutana na mwenzake wa Indonesia
2022-07-27 08:52:04| CRI

Rais Xi Jinping wa China jumanne alasiri alifanya mazungumzo na mwenzake wa Indonesia Joko Widodo katika Jumba la Wageni la Ikulu la Diaoyutai mjini Beijing.

Kwenye mazungumzo yao, viongozi hao wawili wamebadilishana maoni kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa wanayoyafuatilia kwa pamoja na kufikia makubaliano mengi.

Rais Xi amesema, hivi sasa Wachina wako mbioni kuelekea lengo la miaka 100 ya pili ambalo ni kuijenga China kuwa nchi kubwa ya kisasa ya kijamaa, huku watu wa Indonesia wakiwa njiani kutimiza lengo la mwaka 2045. Amesema anapenda kushirikiana na rais Widodo kuendeleza uhusiano wa nchi zao kwa mtazamo wa juu wa kimkakati na maono ya mbali, ili kuwanufaisha zaidi watu wa nchi hizo mbili na kutoa mchango mkubwa zaidi kwenye amani na utulivu wa kikanda na dunia.

Siku hiyo, mke wa rais wa China Bibi Peng Liyuan pia alikutana na mwenzake wa Indonesia Bibi Iriana Joko Widodo.