Mwaka huu wa 2022 Jumuiya ya Wanawake Afrika (PAWO) inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake. PAWO ni jumuiya ya kwanza ya wanawake barani Afrika, ambayo imechangia katika mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika kutoka kwa wakoloni, kutokomeza ubaguzi wa rangi na kutokomeza tofauti za kijinsia, ubaguzi dhuluma dhidi ya wanawake.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1962 jijini Dar Es Salaam, Tanzania, mwaka mmoja kabla ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika, dhamira ya PAWO imekuwa ni kuhakikisha kwamba masuala ya wanawake yanajumuishwa katika ajenda ya ukombozi wa Afrika na kwamba wanawake wanashiriki, kwa usawa, kikamilifu na kwa ufanisi, katika mambo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni katika bara hili. PAWO, Shirika Maalum la Umoja wa Afrika, limekuwa na jukumu muhimu katika kuhamasisha wanawake wa Afrika ndani ya bara hilo na Diaspora kupambana kwa pamoja kwa ajili ya kuiweka huru Afrika na kuifanya iwe na ustawi.
Kwa maana hiyo, Afrika inaadhimisha Siku ya Wanawake wa Afrika ifikapo tarehe 31 Julai kila mwaka ili kusherehekea na kuwaenzi Kina mama watangulizi wa Afrika ambao walipigana kwa ushujaa ili kuleta ukombozi na maendeleo ya bara hili. Na leo kwenye kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia mchango mkubwa uliotolewa na wanawake hawa.