Tanzania na UNICEF zazindua kampeni ya kumaliza ndoa za utotoni
2022-07-29 08:54:36| CRI

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) imezindua kampeni inayolenga kumaliza ndoa za utotoni nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na UNICEF jijini Dar es Salaam imesema, kampeni hiyo iliyozinduliwa jumatano wiki hii inayoitwa Binti, inalenga kupata uungaji mkono wa jamii ili kuongeza umri wa msichana kuolewa na kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu umuhimu wa mtoto wa kike.

Taarifa hiyo imesema, kuzuia ndoa za utotoni ni mwanzo wa kukabiliana na masuala mengine makubwa yanayowahusu watoto na matarajio ya vijana na fursa za maisha, thamani ya wasichana katika jamii, kuvunja mzunguko wa umasikini, na kuhakikisha nafasi za vijana kama wakala wa mabadiliko.

Inakadiriwa kuwa, wasichana watatu kati ya 10 nchini Tanzania wanaolewa wakiwa bado watoto, na kuifanya nchi hiyo kushika nafasi ya 11 kwa ndoa za utotoni duniani.