China yasema endapo Pelosi atatembelea Taiwan jeshi halitakaa tuli
2022-08-02 09:44:49| CRI

Kwa mara nyingine tena China imeionya Marekani kwamba kama Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi atatembelea Taiwan, jeshi laChina halitakaa tuli na litachukua hatua kali na thabiti za kulinda mamlaka ya nchi.

Onyo hilo lilitolewa jana Jumatatu na msemaji wa wizara ya mambo ya nje Zhao Lijian ambaye alisisitiza kwamba China imeikumbusha tena na tena Marekani juu ya wasiwasi wake mkubwa kuhusu suala hili, na msimamo wake wa kupinga vikali ziara ya Pelosi kisiwani Taiwan, pia imetilia mkazo matokeo yake mabaya kama Pelosi atatembelea Taiwan.

Bw. Zhao amesema wale wanaochezea moto basi mwisho utawaangamiza, na kwamba inaaminika kuwa Marekani imeupata vizuri ujumbe wa wazi na mkali wa China.

Bw. Zhao ameeleza kuwa China inafuatilia kwa karibu safari ya Pelosi, kwani itasababisha uingiliaji mkubwa wa mambo ya ndani ya China, kudhoofisha vibaya mamlaka na ukamilifu wa ardhi, kuvuruga kanuni ya China moja, kutishia amani na utulivu wa mlango bahari wa Taiwan, kudhoofisha vibaya uhusiano wa China na Marekani na kusababisha hali mbaya na matokeo ya hatari.