Serikali ya mpito ya Sudan Kusini yaongezewa muda wa miaka miwili
2022-08-05 09:05:07| CRI

Vyama vinavyounda serikali ya umoja nchini Sudan Kusini vimeiongezea muda wa miaka miwili serikali ya mpito, ambapo Rais Salva Kiir amesisitiza kuwa utawala wake hauongezwi muda ili kuendelea kubaki madarakani, bali ni kwa ajili ya kuiandaa nchi kwa uchaguzi na kubadilishana madaraka kwa amani.

Akiongea baada ya kusaini mwongozo wa uendeshaji wa uchaguzi na kuiongeza muda serikali, rais Salva Kiir alisema wameamua kuandaa udongo kwa kipindi cha miezi 24 ijayo ili kupanda mbegu za uchaguzi wa Sudan Kusini, wakiwa na jeshi la umoja, katiba zenye dira, na uelewa thabiti wa nchi yao, ambao ni kujenga serikali ambayo inaweza kumaliza vita dhidi ya umaskini, ujinga, na kukosa matumaini.

Rais Salva Kiir alitoa wito kwa makundi yanayoshikilia msimamo wao, ambayo hayasaini mkataba wa amani, kujiunga na mchakato wa amani ili kuleta mabadiliko ya amani nchini humo.