Jumuiya ya kimataifa yarejea uungaji mkono wa kanuni ya China moja
2022-08-08 08:56:52| CRI

Jumuiya ya kimataifa imepinga vikali ziara iliyofanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi kisiwani Taiwan nchini China, huku ikirejea tena ahadi yake ya kuheshimu kanuni ya China moja.

Waziri wa Nchi anayeshughulika na Uhusiano wa Kimataifa wa Uganda Okello Oryem amesema, nafasi ya Uganda iko wazi, kwamba itaendelea kushikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja, ambayo ni msingi wa uhusiano kati ya Uganda na China.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon Abdallah Bou Habib  alipokutana na Bw. Qian Minjian, balozi wa China nchini humo,  alisema kuwa nchi yake inaunga mkono mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi wa China na umuhimu wa kuheshimu kanuni ya kuwepo kwa China moja.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Al-Sadiq amesema katika taarifa yake baada ya kukutana na balozi wa China nchini humo Ma Xinmin kuwa, nchi hiyo inaunga mkono juhudi za China katika kulinda mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi yake.

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi naye amesisitiza kuwa, sera ya Misri kuhusu suala la Taiwan imekuwa thabiti na haijabadilika. Amesema Misri inashikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja na inaamini kuwa, kanuni hiyo inasaidia kudumisha usalama na utulivu wa dunia.