Waziri wa mambo ya nje wa China alisema Marekani imefanya makosa matatu juu ya suala la Taiwan
2022-08-08 08:57:07| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema, Marekani imefanya makosa makubwa matatu kufuatia ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi kisiwani Taiwan.

Akizungumza kuhusu mvutano uliopo sasa kati ya China na Marekani wakati wa ziara yake nchini Bangladesh, Wang Yi amesema jambo la kwanza ni kwamba Marekani imeingilia kati mambo ya ndani ya China, na kuongeza kuwa licha ya pingamizi na malalamiko ya China, Marekani iliendelea na mpango wake na kumruhusu Pelosi kufanya ziara Taiwan.

Amesema jambo la pili ni kwamba Marekani inachochea na kuunga mkono nguvu zinazotaka “Taiwan ijitenge”, na kusema kila nchi inalazimika kulinda umoja wa kitaifa na kutoruhusu viasharia vya ufarakanishaji kutowajibishwa.

Pia Wang Yi amesema, Marekani kwa makusudi imeharibu amani katika mlango bahari wa Taiwan.

Amesema  jumuiya ya kimataifa inapaswa kufikia maafikiano ya wazi zaidi na kutoa sauti kubwa zaidi ili kusimamia utaratibu wa kimsingi wa uhusiano wa kimataifa na sheria za kimataifa, na kulinda haki na maslahi halali ya nchi zote zinazoendelea.