Msomi wa Mali: Safari ya Nancy Pelosi kisiwani Taiwan ni uchokozi mtupu dhidi ya China
2022-08-09 10:11:03| CRI

Safari ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani Bibi Nancy Pelosi kisiwani Taiwan, China si kama tu imechochea hasira kubwa za watu wa China, bali pia imepingwa kwa kauli moja na  jumuiya ya kimataifa. Mwanadiplomasia mkongwe na mtaalamu wa masuala ya kimataifa wa Mali Prof. Yoro Diallo, hivi karibuni alipohojiwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG amesema safari ya Bibi Pelosi kisiwani Taiwan ni uchokozi mtupu dhidi ya China, na pia ni tishio kwa amani na utulivu wa kikanda.

Prof. Diallo ambaye pia ni mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, anaona tangu serikali ya Marekani chini ya Rais wa zamani Barack Obama ianzishe mkakati wa "Pivoti ya Asia (Asian pivot)", amani na utulivu katika eneo la Asia na Pasifiki vimekuwa vikikabiliwa na tishio kubwa. Serikali iliyokuwa chini ya Donald Trump iliitaja China kuwa “mshindani mkuu wa kimkakati”, na serikali ya Rais wa sasa Joe Biden inaendelea kuichukulia China kama “changamoto kubwa ya muda mrefu”. Katika hali hii, Marekani imekuwa ikivuruga amani na utulivu wa kikanda kupitia kufanya luteka za kijeshi na kupigia debe eti “utaratibu wa pande nne”. Marekani kwa upande mmoja inadai kuwa inaendelea kushikilia Sera ya China Moja, lakini kwa upande mwingine inatoa uungaji mkono kwa shughuli za wafarakanishaji wa Taiwan. Prof. Diallo anaona safari ya kichokozi ya Nancy Pelosi inaashiria mkakati wa serikali ya Marekani wa kuidhibiti China.

Prof. Diallo amesema katika miaka mingi iliyopita, tabia ya Marekani ya kujikweza dhidi ya nchi nyingine, ufedhuli, uchokozi na kupenda vita imeionesha dunia kuwa nchi hiyo ni tishio kwa amani ya dunia. Vilivyoletwa na Marekani kwa Iraq, Syria, Yemen, Afghanistan na nchi nyingine nyingi ni machafuko na vifo. Iko siku watu wanaopenda amani na kutetea haki watalazimika kuanzisha mahakama maalumu ya kimataifa, ili kuwafikisha mbele ya sheria wale wanaozusha machafuko na ghasia kote duniani. Prof. Diallo amesisitiza kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani zinatakiwa kuacha tabia ya kufanya umwamba, kuacha kujifanya kuwa “Polisi wa Dunia”, na kuacha kujifanya “Mwalimu wa Haki za Binadamu”.