Upigaji kura wa Kenya waendelea kwa amani
2022-08-09 21:17:38| cri

Leo tarehe 9 Agosti imekuwa ni siku ya uchaguzi mkuu nchini Kenya na wakenya zaidi ya milioni 22 waliosajiliwa wameshiriki zoezi hilo kumchagua rais mpya, magavana, maseneta, mwakilishi wa wanawake, wabunge na wakilishi wa wadi.

Mapema leo mamilioni ya wapiga kura walimiminika kwenye vituo zaidi ya 26,000 kote nchini humo kushiriki uchaguzi huo mkuu.

Waangalizi wa nje wamesema hadi sasa zoezi hilo limeendeshwa kwa njia ya amani.

Ronald Mutie anaripoti kutoka Nairobi.

Waangalizi wa uchaguzi mkuu tuliozungumza nao wanasema zoezi hilo limeendelea vizuri na wanatumai kuwa hakutakuwa na hitilafu kuanzia sasa hadi matokeo yatakapotangazwa.

Huyu hapa ni aliyekuwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye ni Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Taasisi ya Uchaguzi ya Demokrasia Endelevu Barani Afrika (EISA).

“Nimefurahishwa na kile nilichokiona. Nimeshiriki uangalizi wa chaguzi nyingi na naweza kusema nimependezwa na matayarisho ya Kenya kwenye uchaguzi mkuu huu. Tungependa mambo yaendelee hivyo hivyo hadi wakati wa kuhesabiwa kwa kura.”

Naye Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete, anaongoza ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kila kitu kimekwenda vizuri, kuna amani ya kutosha na utulivu wa kutosha, tunaomba iende hivyo mpaka mwisho wa uchaguzi na baada ya hapo Kenya ibaki kuwa nchi ya amani.”

Vituo vilifunguliwa tangu saa kumi na mbili alfajiri na wapiga kura wamemchagua Rais, Gavana, Seneta, Mwakilishi wa wanawake, wabunge na wawakilishi wa bunge kaunti.

Felix Juma mwenye umri wa miaka 22 anapiga kura kwa mara ya kwanza.

“Nimefurahi kupiga kura kwa mara ya kwanza, nimekuwa nikingojea sana kufanya hivyo naona kuna utulivu.”

 Kumekuwa na hitilafu na baadhi ya mitambo ya kutambua wapiga kura kielektroniki lakini tume ya uchaguzi imeidhinisha kutumika kwa sajili ya vitabu.

Juliana Cherera, ni naibu mwenyekiti wa tume hiyo.

“Tume ya uchaguzi kupitia maafisa wake wa tehama inatatua hitilafu zote za mitambo ya kupigia kura kwa njia ya kielektroniki ambazo zimeripotiwa na maafisa wetu wa kusimamia uchaguzi katika maeneo kadhaa nchini. Tume imeruhusu maeneo yaliyoathirika kutumia sajili ya vitabu kuwatambua wapiga kura. Baadhi ya maeneo yaliyoruhusiwa kutumia sajili ya vitabu ni eneo bunge la Kibwezi Magharibi katika kaunti ya Makueni, lenye vituo 84 vya kupigia kura. Vile vile, baadhi ya maeneo bunge ya  kaunti ya Kakamega kama vile Malava, Matungu, Mumias Magharibi na Mumias Mashariki pia yanatumia sajili ya vitabu kuwatambua wapiga kura.”

Kuhesabiwa kwa kura kunaanza pindi tu zoezi la upigaji kura linapokamilika saa kumi na moja jioni.