China yatoa wito wa kuzisaidia nchi zinazoendelea kuongeza uwezo wa kupambana na ugaidi
2022-08-10 08:42:18| CRI

Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Zhang Jun ametoa wito wa kuzisaidia nchi zinazoendelea haswa zile za Afrika kuongeza uwezo wa kupambana na ugaidi.

Balozi Zhang alisema hayo alipohutubia Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani na usalama wa  kimataifa.

Pia amesema mashirika ya kupambana na ugaidi ya Umoja wa Mataifa ikiwemo Kamati ya Kupambana na Ugaidi ya Baraza la Usalama inatakiwa kuweka mkazo katika kutoa rasilimali nyingi zaidi kwa ajili ya ujenzi wa uwezo wa kupambana na ugaidi, kuunga mkono nchi zinazoendelea kuongeza uwezo wa kupambana na ugaidi katika mambo ya utungaji wa sheria, usimamizi na utekelezaji wa sheria. Ameongeza kuwa, wakati nchi za nje ya kanda hiyo zinaporekebisha uwekaji wa vikosi vya kijeshi barani Afrika, zinatakiwa kuimarisha uratibu na nchi za Afrika, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo  katika wakati wa kupambana na ugaidi chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.