Biashara ya mtandaoni inavyowanufaisha wanawake
2022-08-12 08:30:02| CRI

Biashara ya mtandaoni au maarufu ‘digital business’ ni aina ya teknolojia iliyopo sasa na imebadili mfumo wa biashara wa awali uliowahitaji muuzaji na mnunuzi kuonana. Sasa ni mfumo wa biashara unaomruhusu muuzaji na mnunuzi kufanya biashara, wakiwa katika maeneo tofauti. Teknolojia hiyo, pia imeongeza thamani ya biashara kwa kuzingatia kuwa imeweza kurahisisha shughuli za kila siku za biashara, kuongeza wigo wa masoko na kuongeza ufanisi wa kuhudumia wateja. Nchi zinazoendelea zikiwemo Kenya na Tanzania, zinaonyesha kuongoza kwa ongezeko kubwa la watumiaji wa mitandao.

Wastani wa utumiaji mtandao kidunia, unatajwa kuwa saa saba kwa kila mtumiaji kwa siku na taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mwaka 2020, zinaonyesha kuna jumla ya watumiaji mitandao milioni 27, Tanzania ikiwa na ongezeko la watumiaji zaidi ya milioni moja tangu mwaka 2019. Lingine katika hilo, kuna suala la kuongezeka idadi ya watumiaji wa mitandao hiyo kwenye soko la mtandao, idadi kubwa ya watumiaji wanapata nafasi kupitia bidhaa mbalimbali zinazowekwa na wafanyabiashara katika mitandao. Hivyo leo hii tukiwa tunaongelea biashara ya mtandaoni, kwenye ukumbi wa wanawake tutaangalia biashara hii inawanufaisha vipi wanawake.