Msomi wa Cameroon: Marekani yafanya hila tena kwenye suala la Taiwan
2022-08-11 15:49:13| CRI

Wimbi la lawama dhidi ya safari ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani Bibi Nancy Pelosi kisiwani Taiwan, China bado linaendelea kusambaa. Msomi wa masuala ya kimataifa wa Cameroon Dkt. Taling Tene Rodrigue, hivi karibuni alipohojiwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG amesema kitendo hicho cha Bibi Pelosi kimeionesha dunia mara nyingine tena sura halisi ya ulaghai wa serikali ya Marekani.

Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Nchi zinazotumia Kifaransa katika Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, Dkt. Taling Rodrigue amesema, wakati rais Joe Biden wa Marekani alipozungumza na Rais Xi Jinping wa China kwa njia ya simu tarehe 28 Julai, alisisitiza tena kuwa Marekani haijabadili na haitabadili sera yake ya kuwepo kwa China moja, na wala haiungi mkono Taiwan kujitenga na China. Mbali na hayo, pia kuna wanasiasa na wasomi wengi wa Marekani walioeleza wazi kupinga safari hiyo ya Nancy Pelosi kisiwani Taiwan. Katika hali hii, Bibi Pelosi akiwa ni kiongozi wa tatu kwenye ngazi ya madaraka nchini Marekani, alishikilia kuendelea na safari hiyo kwa kupanda ndege ya kijeshi, kitendo ambacho ni uingiliaji wa wazi katika mambo ya ndani ya China, na kimekiuka vibaya mamlaka ya China na ukamilifu wa ardhi yake.

Dkt. Rodrigue amesema serikali ya Marekani inajulikana kwa sifa mbaya ya ulaghai na kutokuwa na uaminifu. Serikali ya Marekani ilitoa ahadi wazi kwenye taarifa ya pamoja ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati yake na China, kuwa Marekani inaitambua Jamhuri ya Watu wa China kuwa ni serikali pekee halali ya China, na watu wa Marekani watakuwa na uhusiano usio rasmi tu, ukiwemo wa kiutamaduni na kibiashara, na upande wa Taiwan. Lakini Dkt. Rodrigue anaona ni wazi kwamba safari hiyo ya Pelosi kisiwani Taiwan si mawasiliano yasiyo rasmi kama iliyoahidi, bali inaonesha kwa mara nyingine tena kuwa Marekani imefanya hila kwenye suala la Taiwan.

Dkt. Rodrigue amebainisha kuwa kwa upande mmoja serikali ya Marekani inasisitiza kufuata sera ya China Moja, kwa upande mwingine inapuuza dhamira thabiti ya watu wa China ya kulinda mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi yao na kumwacha Bibi Nancy Pelosi afanye safari ya kiuchokozi kisiwani Taiwan, je, huu sio ni ulaghai wa hali ya juu kabisa? Mpaka sasa, jumla ya nchi 181 kote duniani zimeanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Jamhuri ya Watu wa China katika msingi wa kanuni ya China Moja, na kanuni hiyo pia ni msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Marekani. Dkt. Rodrigue amesisitiza kuwa kama Marekani inapuuza kwa makusudi ahadi hizo za kisiasa zilizoko kwenye nyaraka, basi jumuiya ya kimataifa inabidi kuikumbusha.