Tanzania yatoa huduma ya internet ya kasi kwenye mlima Kilimanjaro
2022-08-17 08:27:06| CRI

Shirika la simu la Tanzania TTCL limeweka huduma ya internet ya kasi kwenye kilele cha Horombo cha Mlima Kilimanjaro kupitia mradi wa taifa wa mkonga wa mawasiliano.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tehama wa Tanzania Bw. Nape Nnauye amesema sasa watalii wanaweza kuwasiliana na sehemu mbalimbali duniani wakiwa kwenye kilele cha mlima huo.

Mradi wa mkonga wa mawasiliano wa taifa una lengo la kuhimiza matumizi ya Tehama kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na serikali mtandao, elimu mtandao, afya mtandao, biashara mtandao na mengine mengi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Bw. Nnauye amesema huduma ya Internet pia inatarajiwa kufikishwa kwenye kilele cha Uhuru ifikapo mwezi Oktoba.