Marekani yasafirisha zaidi mafuta yaliyoibwa Syria hadi kwenye kambi zake nchini Iraq
2022-08-22 10:23:57| CRI

Shirika la habari la Syria SANA limeripoti kuwa vikosi vya Marekani jana Jumapili vilisafirisha zaidi mafuta yaliyoibwa kwenye visima vya mafuta kaskazini mashariki mwa Syria na kuyapeleka hadi kwenye kambi zake nchini Iraq yakiwa yamebebwa kwenye msafara wa magari 137 ya mafuta, chini ya msaada wa kundi la wapiganaji la SDF linaloongozwa na Wakurdi.

Pamoja na usafirishaji huo mpya, tangu Agosti 11 Marekani imechukua jumla ya magari 535 ya mafuta yaliyoibwa Syria .

Serikali ya Syria imeishutumu Marekani kwa kuiba maliasili nchini Syria, kama vile mafuta, gesi na ngano.

Agosti 8, Wizara ya Mafuta ya Syria ilisema katika taarifa yake kwamba Marekani na mamluki wake wanaiba wastani wa mapipa 66,000 ya mafuta kwa siku nchini Syria, karibu asilimia 80 ya uzalishaji wa mafuta nchini humo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa wizi huo wa mafuta wa muda mrefu umeitia Syria hasara ya dola za kimarekani bilioni 105.