Kenya yasema idadi ya watu wenye ukosefu wa chakula itapanda kutokana na ukame mkali
2022-08-22 10:20:11| CRI

Idadi ya Wakenya wenye ukosefu wa chakula inatarajiwa kufikia milioni 4.35 hadi ifikapo Oktoba mwaka huu, idadi ambayo itakuwa juu zaidi ikilinganishwa na ya hivi karibuni ambayo ni milioni 4.1, huku ukame ukizidi kuwa mkali zaidi katika sehemu nyingi za nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Taifa ya Kuzuia Ukame (NDMA) iliyotolewa jijini Nairobi, kaunti 23 nyingi zikiwa za mikoa kame na nusu ukame zinakumbwa na ukame mkali ambao umesababisha ukosefu wa maji, baa la njaa na utapiamlo. Hali mbaya ya ukosefu wa chakula inachangiwa na uhaba wa mvua katika msimu wa nne mfululizo pamoja na athari nyingine kama vile mzozo wa Ukraine, nzige wa jangwani na janga la UVIKO-19.

Hared Hassan Adan, Afisa Mtendaji Mkuu wa NDMA amesema mwezi Agosti pekee, asilimia 95 ya ardhi kame na nusu kame zitakuwa kavu zaidi, na kuwafanya wafugaji na wakulima kukumbwa na njaa na utapiamlo.