Umuhimu wa afya ya mama na mtoto kuanzia njia zinazotumika kuzalisha mtoto hadi makuzi yake
2022-08-26 08:30:03| CRI

Kuanza tabia za kujali afya njema ili kuzuia magonjwa sugu ni rahisi na zinakuwa na ufanisi zaidi wakati wa utoto na ujana kuliko kujaribu kubadilisha tabia mbaya wakati wa utu uzima. Takwimu za shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa mwaka 2020 pekee, watoto milioni 149 duniani walio na umri chini ya miaka 5 wana ukuaji hafifu huku milioni 38.9 wakiwa na unene uliopita kiasi. Kila mwaka, asilimia 45 ya vifo vyote vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 vinavyotokea duniani huhusishwa na lishe duni. Changamoto hii huonekana zaidi kwenye nchi masikini duniani, pamoja na zile zenye uchumi wa kati.

Ili kujali afya bora ya mtoto chakula ndiyo msingi mkuu wa kubadilisha kila kitu. Kwa kutambua umuhimu huu, wataalamu wa vyakula na lishe wameweka mgawanyo wa makundi matano ya vyakula, ambayo ni pamoja na vyakula vya asili ya nafaka, mizizi, ndizi mbichi. Vyakula asili ya wanyama na jamii ya mikunde. Mbogamboga Matunda Sukari, mafuta na asali. Ili mtu awe na afya bora, anapaswa kuhakikisha kuwa mlo wake wa kila siku unajumuisha makundi haya tajwa nah ii ikiwa ni pamoja na watoto wadogo kwa watoto wachanga wao wana utaratibu wao maalumu unaohusiana moja kwa moja na na maziwa ya mama.

Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu unyonyeshaji unaelekeza wanawake wanyonyeshe watoto wao kwa angalau miaka 2, huku miezi 6 ya mwanzo ikihusisha maziwa pekee ya mama pasipo kuchanganya vyakula vingine, au hata maji ya ziada kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya maziwa ya mama ni maji.

Muongozo huu umekuwa haufuatwi ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kukosekana kwa uelewa, kutunza urembo wa maungo hasa matiti kwa kigezo cha kuogopa kuyaharibu pamoja na kukosekana kwa muda wa kutosha kulea watoto kutokana na sababu zinazotajwa kuwa za kujikwamua kiuchumi. Matokeo yake, watoto wengi wamekuwa hawanyonyeshwi ipasavyo, na wengine wengi wamekuwa wahanga wa kuanzishiwa vyakula mbadala mapema, kabla hata hawajafikisha

Ili kujua namna gani ya kumtunza mtoto awe na afya bora pamoja na kujali afya mama, katika kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake leo tutazungumzia umuhimu wa afya ya mama na mtoto kuanzia njia zinazotumika kuzalisha mtoto hadi makuzi yake.