Wadau wa internet wa Afrika wajadili njia za kuboresha muunganisho wa mtandao
2022-08-25 09:30:43| CRI

Kongamano la wadau wa internet lilifunguliwa Jumatano ya wiki hii mjini Kigali Rwanda likiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha muunganisho wa mtandao wa nchi hiyo na bara zima.

Akifungua kongamano hilo lijulikanalo kama “Jukwaa la Kuangalia na Kuunganisha Afrika (AfPIF)” Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvumbuzi na TEHAMA wa Rwanda, Yves Iradukunda amesema upatikanaji na matumizi ya mtandao mpana wa internet una ushawishi mkubwa katika kuboresha ufikishaji wa huduma katika sekta ya uchumi, akibainisha kuwa hivi sasa matumizi ya internet yanaleta matokeo mazuri katika kujifunza, kufikisha huduma za afya, kusimamia vizuri rasilimali za nishati, na kuwezesha wananchi kuwasiliana na serikali.

Naye mwanateknolojia wa Jamii ya Internet Michuki Mwangi amesema maendeleo makubwa yamefikiwa katika kuanzisha Maeneo Mapya ya Mabadilishano ya Internet (IXPs), huku yakisaidia ukuaji wa yale yaliyopo. Mwangi ametaja umuhimu wa kuzidisha ushirikiano kati ya watoaji huduma za internet, makampuni ya mtandao wa simu, watoaji wa maudhui, mtandao wa makampuni makubwa, na watunga sera.