Somalia na mashirika ya UM yaongeza juhudi za kutoa chanjo ya COVID-19
2022-08-29 09:02:30| CRI

Somalia na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa zimeahidi kuongeza juhudi za kutoa chanjo ya COVID-19 nchini humo, licha ya ukame mkali unaokumba maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Wizara ya Afya ya Somalia kwa pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) imesema baadhi ya changamoto zinazopunguza kasi ya utoaji wa chanjo ya COVID-19 nchini humo ni pamoja na kutofikiwa kwa baadhi ya maeneo maalum kutokana na ukosefu wa usalama ama changamoto za kiugavi.

Katika taarifa yao ya pamoja, waziri wa Afya na Huduma za Jamii nchini Somalia Ali Haji Adam Abubakar amesema, chanjo zilizopokelewa na Wizara yake zitaokoa maisha, kuwawezesha kuleta usawa kati ya Wasomali wa maeneo mbalimbali, na kuchangia katika malengo ya taifa ya afya.

Naye Mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia Wafaa Saeed Abdelatif amesema, hali ya kibinadamu inahitaji hatua za haraka ili kuongeza utoaji wa chanjo ya COVID-19 na misaada mingine ya kuokoa maisha, hususan kwa wakimbizi wa ndani, jamii za vijijini, na wafugaji wanaohamahama. Amesema UNICEF itaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Somalia na wenzi wake ili kuhakikisha jamii zinafahamu umuhimu wa chanjo hiyo.