Kwa muda mrefu wanaume nchini Kenya waling’aa kwenye nyadhifa za uongozi huku wakichaguliwa kwa wingi zaidi ila kwa upande wa wanawake walikuwa wakichaguliwa wachache mno hadi ilipofika mwaka 2010 wakati katiba mpya ya Kenya ilipoagiza kwamba theluthi moja ya nyadhifa za uongozi zitengwe kwa ajili ya watu wa jinsia moja ambayo kwa wakati huo ililenga kina mama. Ili kusaidia kutimiza hitaji hilo, kulibuniwa wadhifa wa mwakilishi wa kike wa kaunti bungeni huku wengine wachache wakichaguliwa kwenye nyadhifa za kumenyana na wanaume.
Kwa hiyo katika uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka huu uliomalizika hivi majuzi, Wanawake wengi zaidi wamegombea nyadhifa za uongozi na kushinda ikilinganishwa na ule uliopita, haya yakiwa ni matokeo ya juhudi za mashirika ya serikali kufanya kazi pamoja katika kuboresha mazingira wezeshi ya kisiasa kwa wagombea wanawake. Hivyo leo kwenye kipindi cha ukumbi wa wanawake tutaangalia wanawake wa Kenya walivyoleta mageuzi katika uchaguzi mkuu pia wanawake wanaoshikilia nyadhifa za juu kabisa.