WHO yasema dawa za jadi ni muhimu katika kupunguza mzigo wa magonjwa Afrika
2022-09-01 08:31:45| CRI

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Bi. Matshidiso Moeti amesema, nchi za Afrika zinapaswa kuboresha dawa za jadi zilizothibitisha ufanisi katika kusimamia na kutibu magonjwa yanayowaathiri watu wa bara hilo.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana jijini Nairobi, Kenya, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Dawa za Asili za Afrika kwa mwaka huu, Bi. Moeti amesema dawa hizo zinaaminika, zinakubalika, ni za bei nafuu na ni chanzo cha huduma za afya kwa Waafrika kwa karne kadhaa.

Amesema asilimia 80 ya idadi ya watu barani Afrika wanategemea dawa za jadi kwa mahitaji yao ya afya ya kimsingi, na kuongeza kuwa, bara hilo limetoa kipaumbele kwa maendeleo ya dawa hizo kupitia utungaji wa sera, utafiti na mafunzo.

Amesema katika miongo miwili iliyopita, bara hilo limetunga mikakati ili kuingiza dawa za asili katika program za kitaifa za huduma ya afya.