Serikali zinavyosaidia vijana kupata ajira
2022-09-08 08:30:41| CRI

Kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 24 ambacho kimekuwa kikiongezeka sana duniani kinaleta changamoto kubwa kwa hivi sasa. Mwaka 2020, kilipungua kwa asilimia 8.2 kote duniani. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya Kamisheni ya Ulaya, mwaka 2021 kiwango cha vijana wasiokuwa na ajira barani Ulaya kilipanda hadi asilimia 16.6. Vijana ndio kundi la watu wanaoathirika vibaya zaidi kwa kupoteza kazi katika kipindi cha janga la UVIKO-19.

Ripoti mpya ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) iliyotolewa Agosti 11 kwa lengo la kusherehekea siku ya vijana duniani iliyofanyika Agosti 12 inasema suala la vijana kupata ajira tena na kujikwamua na hali ngumu ya maisha baada ya janga la ugonjwa wa COVID-19 limeendelea kusuasua, ambapo shirika hilo linasema hali hiyo inathibitisha kuwa COVID-19 iliathiri zaidi vijana kuliko marika mengine, vijana wa kike ndio walioathirika zaidi, ambapo ripoti hiyo inaonesha kuwa mwaka huu wa 2022 makadirio ya vijana wa kike watakaokuwa kwenye ajira ni asilimia 27.4 ikilinganishwa na vijana wa kiume asilimia 40.3. Hii ina maana vijana wa kiume wana nafasi mara 1.5 ya kuajiriwa kuliko vijana wa kike. Pengo la kijinsia ambalo limeonesha dalili ndogo sana kuzibika katika miongo miwili iliyopita, sasa limekuwa kubwa zaidi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ikilinganishwa na zile za kipato cha juu. Hivyo kutokana na changamoto hiyo leo katika Ukumbi wa Wanawake tutaangazia namna serikali zinavyosaidia vijana wake wakiwemo vijana wa kike kupata ajira na kuweza kujikwamua kimaisha.