Tanzania kutumia dawa za jadi katika hospitali za rufaa
2022-09-06 09:19:27| CRI

Mamlaka za afya za Tanzania zimesema kuna mpango wa kutumia dawa za jadi katika hospitali za rufaa zinazoendeshwa na serikali nchini Tanzania.

Waziri wa afya wa Tanzania Bibi Ummy Mwalimu amesema matumizi ya dawa za jadi yataanzishwa kama mradi wa majaribio. Serikali imeanza kutoa huduma ya dawa hizo katika Kituo cha Afya cha Momela huko Meru na Kituo cha Maibong-Suki huko Dar es Salaam.

Bibi Mwalimu ameongeza kuwa serikali imeweka sera husika kuhusu dawa za jadi huku vyuo vikuu vingi vya serikali vikifanya uchunguzi kuhusu ufanisi wa dawa hizo. Amesema ufanisi wa dawa hizo ulizingatiwa wakati wa janga la COVID-19 ambapo baadhi zilisaidia kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo. Pia amedokeza kuwa serikali inajenga kiwanda cha kuchakata dawa za jadi huko Mabibo mjini Dar es Salaam.