Msomi wa Cameroon: “Mazungumzo ya Tiangong”yaakisi mustakbali mzuri wa ushirikiano kati ya Afrika na China kwenye sekta ya anga ya juu
2022-09-13 08:54:01| CRI

Tarehe sita mwezi Septemba, Tume ya Umoja wa Afrika, Ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika na Ofisi ya Miradi ya Kupeleka Wanaanga Kwenye Anga ya  Juu ya China walifanya kwa pamoja shughuli ya “Mazungumzo ya Tiangong” ambapo wanaanga wa China walioko katika kituo cha anga ya juu cha Tiangong waliwasiliana moja kwa moja na kujibu maswali  waliyotoa vijana wa Afrika kwa njia ya video. Msomi wa masuala ya kimataifa wa Cameroon Dkt. Taling Tene Rodrigue alitazama matangazo ya moja kwa moja ya shughuli hiyo kutoka kwenye Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Piili cha Yaoundé. Akihojiwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, Dkt. Rodrigue alisema ameona mustakbali mzuri wa ushirikiano kati ya Afrika na China kwenye sekta ya anga ya juu  kwa kupitia shuguli hiyo ya “Mazungumzo ya Tiangong”.

Dkt. Rodrigue, ambaye pia ni naibu mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa nchi zinazotumia lugha ya Kifaransa cha Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, amesema sekta ya anga ya juu barani  Afrika bado iko katika hatua ya mwanzo, ambapo nchi za Afrika kwa sasa zinadhibiti satelaiti 41, idadi ambayo inachukua asilimia moja  tu ya satelaiti zote zinazofanya kazi kwenye mzunguko wa dunia. Anaona, ukosefu wa uwezo katika sekta ya anga ya juu pia ni  vizuizi kwa Afrika kufikia Malengo ya Maendeleo Eendelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030. Umoja wa Afrika umepitisisha mkakati wa anga ya juu, ili kuziwezesha nchi za Afrika kutumia fursa zinazotokana na safari za anga ya juu na matumizi ya teknolojia za anga ya juu. Amesema, sekta ya anga ya juu imekuwa nyanja muhimu kwenye ushirikiano kati ya Afrika na China.

Dkt. Rodrigue amesema nchi za Afrika zikiwemo Ethiopia, Algeria, Misri na Namibia zimeanza kuendeleza sekta ya anga ya juu kutokana na uungaji mkono wa China kwa hatua mbalimbali halisi kama vile urushaji wa satelaiti na ujenzi wa miundombinu ya anga ya juu  . Ameongeza kuwa, “Mazungumzo ya Tiangong” ni mfano mmoja tu wa ushirikiano kati ya Afrika na China kwenye sekta ya anga ya juu katika zama mpya, na China inajithibitisha kivitendo kuwa ni mwenzi wa kutegemeka kwa nchi za Afrika katika siku zijazo.

Dkt. Rodrigue amesema, Cameroon kwa sasa inafanya upembuzi yakinifu kuhusu mpango wake wa anga ya juu, na kushirikiana na China ni fursa nzuri kwa Cameroon kusukuma mbele mpango wake kwenye sekta hiyo. Anatarajia kuwa kutokana na misaada ya China, Cameroon itajiunga mapema  katika nchi za Afrika zenye satelaiti.