Rais Xi Jinping atoa Makala kabla ya ziara zake nchini Kazakhstan na Uzbekistan
2022-09-14 10:28:29| CRI

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya China, rais Xi Jinping atahudhuria mkutano wa 22 wa viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) mjini Samarkand, na kufanya ziara ya kiserikali nchini Kazakhstan na Uzbekistan kuanzia tarehe 14 hadi 16 mwezi Septemba. Ziara hizo zinafanyika kutokana na mwaliko wa wenzake wa Jamhuri ya Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev na wa Jamhuri ya Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev.

Kabla ya ziara yake, rais Xi alitoa makala mbili moja katika gazeti la Kazakhstanskaya Pravda yenye kichwa kisemacho “Kujenga Mambo ya nyuma ili kupiga hatua zaidi katika ushirikiano baina ya China na Kazakhstan” na nyingine katika vyombo vya habari vya Uzbekistan isemayo “Kushirikiana pamoja kwa ajili ya Mustakabali mzuri wa uhusiano kati ya China na Uzbekistan.”

Kwenye Makala aliyotoa nchini Kazakhstan rais Xi amesema mwaka huu ikiwa China na Kazakhstan zinaadhimisha miaka 30 ya uhusiano wa kibalozi, katika miongo mitatu iliyopita wamekabiliana kwa ujasiri na mitihani yote huku wakishikana mikono pamoja.

Ameeleza katika ziara yake atakuwa na mazungumzo ya kina na rais Tokayev juu ya kuendeleza zaidi ushirikiano wa kudumu na kimkakati kati ya China na Kazakhstan na kuboresha zaidi ushirikiano wa kunufaishana kwa pande zote. Pia amesema wataweka mipango ya ushirikiano ili kuhimiza uhusiano baina ya pande mbili pamoja na malengo na dira ya kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Kazakhstan.

Amesisitiza kuwa kwanza wanahitaji kuendeleza ujirani mwema na urafiki na kwamba kuaminiana kwa kina kwenye mambo ya kisiasa ndio msingi wa maendeleo endelevu na thabiti wa uhusiano wa nchi hizo mbili. Jambo la pili amesema wanahitaji kuongeza zaidi ushirikiano wa kunufaishana kwa kuboresha uwekezaji na uwezeshaji wa biashara, kufungua mipaka ya bandari na usafirishaji wa kuvuka mipaka na kuandaa vyanzo vipya vya ukuaji kama vile akili bandia, big data, fedha za kidijitali, biashara kwenye mtandao na nishati ya kijani. Mwisho pia ametaka nchi hizo mbili ziimarishe uratibu wa kimataifa katika nyanja zote ndani ya miongozo kama vile ya UM, SCO, CICA, na China+Asia ya kati.

Kwa upande wa Makala ya Uzbekistan rais Xi pia amesema China na Uzbekistan mwaka huu zinaadhimisha miaka 30 ya uhusiano wa kibalozi, ambapo katika miongo mitatu iliyopita mti mkubwa wa uhusiano wao umekita mizizi na umekuwa hai zaidi. Hivyo amesisitiza kwamba kwanza wanahitaji kuzidi kuungana mkono na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana, pili wanahitaji kuimarisha uhusiano wa kunufaishana ili kupata maendeleo ya pamoja na ustawi. China inatarajia kushirikiana na Uzbekistan kutekeleza Mpango wa Maendeleo Duniani na kuchukua hatua madhubuti katika kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea na kukuza usawa, uratibu na mazingira ya maendeleo jumuishi ambayo yatakuwa ya ushirikiano wa kunufaishana utakaofanya kazi kwa wote na kuleta ustawi wa pamoja. Mwisho amesema wanahitaji kukuza mawasiliano ya kiutamaduni na kuongeza maingiliano baina ya mtu na mtu.