Rais Xi afanya mazungumzo ya kina na mwenzake Tokayev wakati akiwa ziarani nchini Kazakhstan
2022-09-15 09:43:40| CRI

Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na mwenzake Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan wakati alipokuwa ziarani Jamhuri ya Kazakhstan Jumatano mchana.

Katika mazungumzo yao rais Xi amesema China na Kazakhstan zimeanzisha uhusiano wa kibalozi kwa zaidi ya miongo mitatu, ambapo uhusiano wa pande mbili umeshinda majaribu ya kubadilika kwa mazingira ya kimataifa, kupata mafanikio makubwa, kufikia ngazi za juu na kuleta matokeo mazuri.

Amesema nchi mbili zimekuwa wa kwanza kufanya mambo mengi kwenye uhusiano wao, yakiwemo kuwa wa kwanza katika kutuliza suala la mpaka, wa kwanza kuweka mabomba ya mafuta na gesi kutoka China hadi Kazakhstan, wa kwanza kufanya ushirikiano wa kimataifa katika kuwezesha uzalishaji na wa kwanza kujenga ushirikiano wa kina wa kudumu na kimkakati.

Pia amesema China inathamini sana uhusiano wake na Kazakhstan katika kulinda uhuru na mamlaka ya nchi, na kuchukua hatua za mgeuzi ili kurejesha maendeleo na utulivu wa taifa na kuongeza kuwa China daima itakuwa rafiki na mshirika anayeaminika na kutegemeka.

Amebainisha kuwa China iko tayari kushirikiana na Kazakhstan katika kuungana mkono kithabiti kwenye maendeleo na kufufua uchumi, na kusaidiana ili kupata maendeleo na ustawi.

Kwa upande wake rais Tokayev amesema ukweli kwamba rais Xi amechagua kutembelea Kazakhstan katika ziara yake ya kwanza ya nje tangu kuibuka kwa janga la UVIKO-19, na katika tukio la kuadhimisha miaka 30 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Kazakhstan, unaonesha kuwa pande mbili zinaaminiana sana na kwamba ushirikiano wa kudumu na kimkakati baina ya nchi mbili ni wa ngazi ya juu.

Tokayev amesema Kazakhstan itaendelea kushikilia sera ya China moja na kuwa mshirika na rafiki mzuri ambaye China daima anaweza kumtegemea kwenye hali yoyote ile. Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Tokayev amesema pendekezo hili limekuwa injini muhimu ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja, na Kazakhstan itaendelea kuunga mkono kwa nguvu zote na kushiriki kwenye pendekezo hili. Kuhusu suala la UVIKO-19 rais Tokayev ameishukuru China kwa msaada wake wa thamani iliyoupata nchi yake.

Viongozi hao wawili walisaini na kutoa taarifa ya pamoja kati ya China na Kazakhstan kuhusu miaka 30 ya uhusiano wa kibalozi na kutangaza kwamba nchi hizo mbili zitashirikiana kwa lengo na maono ya kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja inayofafanuliwa na urafiki wa kudumu, kuaminiana na kuwa pamoja katika shida na raha. Wakati huohuo rais Xi amepokea nishani ya Tai wa Dhahabu “Altyn Qyran” aliyotunikiwa na mwenyeji wake rais Tokayev.