Rais Xi asema China iko tayari kushirikiana na Russia na kuungana mkono katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi
2022-09-16 08:49:19| CRI

China iko tayari kushirikiana na Russia na kuzidi kuungana mkono kwenye masuala yanayohusu maslahi yao ya msingi.

Hayo yamesemwa jana na rais Xi Jinping wa China wakati alipokutana na mwenzake wa Russia Vladmir Putin huko Samarkand, ambapo pia walibadilishana maoni kuhusu uhusiano wa China na Russia, na masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja. Xi amesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu, nchi hizi mbili zimedumisha mawasiliano ya ufanisi ya kimkakati, ambapo ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali umesonga mbele kwa madhubuti, huku shughuli za mwaka wa mawasiliano ya michezo zikiendelea vizuri, na kuwa na kasi kubwa katika ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, pamoja na mawasiliano baina ya watu wao.

Sambamba na hayo, rais Xi pia amesisistiza kuwa China itashirikiana na Russia ili kuimarisha ushirikiano wa kivitendo katika biashara, kilimo, uunganishaji na maeneo mengine.

Kwa upande wake rais Putin ameutakia mafanikio Mkutano wa 20 wa wajumbe wote wa Chama cha Kikomunisti (CPC) na kusema anaamini kuwa chini ya uongozi wa rais Xi, China itaendelea kupata mafanikio mapya katika uchumi na maendelo ya jamii.