Washukiwa 135 wa uhalifu wakamatwa nchini Tanzania
2022-09-20 08:44:19| CRI

Vijana 135 wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 30 wamekamatwa jijini Dar es Salaam, Tanzania, kwa tuhuma za uhalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema, washukiwa hao wamekamatwa na polisi tangu kuanzishwa kwa operesheni maalum alhamis iliyopita, na kuongeza kuwa, washukiwa hao wamehusika katika vitendo vya uhalifu, ikiwemo wizi wa kutumia silaha.

Jana jumapili, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitangaza kuwa, polisi wamewaua vijana wanne wanaoshukiwa kuwa sehemu ya mnyororo wa wahalifu vijana walioleta hali ya tafakuri katika mji huo wa kibiashara.

Ijumaa iliyopita, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania, Camillus Wambura, alitangaza vita dhidi ya wahalifu hao vijana, ikiwa ni siku moja baada ya Bunge la Tanzania kuitaka serikali kuchukua hatua za dharura kukabiliana na uhalifu unaofanywa na vijana hao, hususan katika maeneo ya mijini.