Nchi za Afrika zachukua tahadhari kufuatia mlipuko wa virusi vya Ebola nchini Uganda
2022-09-23 08:42:29| CRI

Nchi za Afrika ziko katika hali ya tahadhari, huku zikiimarisha upimaji na ufuatiliaji baada ya mlipuko wa virusi vya Ebola kuripotiwa mapema wiki hii nchini Uganda.

Akizungumza katika kikao kilichoitishwa na Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Mkuu wa Idara inayofuatilia virusi hivyo iliyo chini ya Wizara ya Afya ya Uganda, Dr. Henry Kyobe ametangaza jana kuwa, mtu mmoja amefariki na wengine saba kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo na kuongeza kuwa, mlipuko huo huenda ulianza kutokea mwanzoni mwa mwezi Septemba.

Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amesema, maofisa muhimu wamepelekwa katika mpaka wa nchi hiyo na Uganda ulioko magharibi mwa Kenya ili kuweza kutambua kesi zinazoshukiwa kuwa na ugonjwa huo.

Mganga mkuu katika Wizara ya Afya nchini Tanzania Dr. Aifello Sichalwe amesema, wizara hiyo imeweka timu za ufuatiliaji katika mikoa iliyoko hatarini zaidi ya Kagera, Mwanza, Arusha, Mara, Kigoma na Dar es Salaam.